Saturday, 17 August 2013

PONDA SEGEREA

KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda, inadaiwa jana amekamatwa na kupelekwa mahabusu katika Gereza la Segerea, Dar es Salaam.Inadaiwa kuwa, Shekhe Ponda alikamatwa na makachero wa polisi saa chache baada ya kuruhusiwa na daktari wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), ambako alikuwa akipatiwa matibabu ya jeraha alilodai kupigwa risasi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, msemaji wa familia ya Shekhe Ponda, aliyejitambulisha kwa jina la Bw.Isihaka Rashidi alisema ndugu yao alikamatwa na polisi dakika tatu baada ya kupewa ruhusa ya kuondoka MOI."Taratibu za kumkamata ndugu yetu hazikufuatwa...sisi tunaamini makachero wa polisi wamemteka Shekhe Ponda ambaye hali yake bado haikuwa nzuri.
"Kiutaratibu, mimi ndiye niliyepaswa kukabidhiwa mgonjwa wangu (Shekhe Ponda)...polisi wamemchukua bila kubeba dawa zake jambo ambalo hatujui atakuwa salama kiasi gani."Da k i k a t a t u b a a d a y a kuruhusiwa, walikuja polisi na kumwambia uko chini ya ulinzi, wamemchukua na kumpeleka mahabusu Segerea...Shekhe Ponda alishtuka sana aliporuhusiwa hivyo aliomba aongezewe siku mbili ili apate unafuu kidogo lakini daktari alikataa na kusema amemruhusu”.
Alisema karatasi ya ruhusa inaonesha jina la daktari aliyemruhusu anaitwa Swai ambapo Shekhe Ponda alipandishwa kwenye gari aina ya Land Cruser yenye vioo vyeusi chini ya ulinzi mkali na msafara wa magari manne.
"Nilipata taarifa kuwa ndugu yangu amechukuliwa na polisi, nilipofika hapa MOI na kuomba karatasi ya ruhusa ya mgonjwa, niliambiwa kuna bili ya sh. milioni 1.1.
"Uongozi wa MOI ulisema naweza kulipa au kuacha jambo ambalo bado najiuliza kama Shekhe Ponda hatalipa fedha hizi nani anayehusika kulipa deni hili," alisema Bw. Rashidi.
Alisema kitendo hicho kimeishtua familia yao kwani hawaamini kama polisi waliomchukua wana nia njema na mgonjwa wao na mpango wa kumkamata ulikuwepo muda mrefu akiwa MOI.
"Inaonesha wazi Jeshi la Polisi wameshinikiza mgonjwa atolewe kabla ya kupata nafuu ili wamchukue jambo ambalo ni kinyume cha sheria na haki ya mgonjwa," alisema.
Aliongeza kuwa, familia itakabidhi tukio hilo kwa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini ili iweze kutoa uamuzi wake.
Msemaji MOI
Kwa upande wake, Msemaji wa MOI, Bw.Almas Jumaa alikiri kuruhusiwa kwa mgonjwa huyo (Shekhe Ponda) na alipoulizwa kama amepelekwa Segerea, alisema jambo hilo hawezi kulizungumzia kwani lipo nje ya uwezo wake.
Tukio la kukamatwa Shekhe Ponda limemkuta siku moja baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili akiwa kitandani na wakili wa Serikali Mwandamizi Tumaini Kweka, mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hellen Liwa.
Shekhe Ponda anadaiwa kuchochea vurugu sehemu mbalimbali nchini. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 28 mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia askari polisi anayedaiwa kufyatua risasi hewani

katika jaribio la kumkamata Shekhe Ponda, Agosti 10 mwaka huu.Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Msemaji wa jeshi hilo nchini, Advera Senso, alisema jeshi hilo limeunda timu ya uchunguzi wa hali halisi ya tukio hilo kabla na baada ya purukushani zilizosababisha wafuasi wa Shekhe Ponda kurusha mawe na askari polisi kufyatua risasi hewani. 
"Uhalali wa timu kwenda eneo la tukio unatokana na kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi zinazoelekeza kufunguliwa jalada la uchunguzi kwa askari yeyote atakayefyatua risasi iwe kwa bahati mbaya au mazingira yanayomlazimu," alisema.Alisema timu hiyo tayari imeanza kazi na inaendelea vizuri hivyo aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati jambo hilo likiendelea kushughulikiwa kisheria ambapo vurugu, fujo au maandamano yasiyo na tija hayatavumiliwa. Habari hii imeandikwa na Kassim Mahege, Revina John na Frank Monyo

No comments:

Post a Comment