Tuesday, 13 August 2013

Oloya hana hadhi ya kugombewa kiasi hicho

MSIMU mpya wa Ligi ya Bara unaanza Agosti 24. Timu 14 zitashiriki na tayari zimekamilisha usajili zikiwa mkao wa kuanza msimu. Hata hivyo, kuna mambo fulani ambayo nimeyaona yamejitokeza ambayo kwa kiasi fulani yanatia aibu haswa kwa watu wenye fikra chanya.
Ni vitu fulani ambavyo vinafanywa na hizi timu na kwa upande mwingine ni makosa ambayo yanalelewa na shirikisho pamoja na kamati zake. Mambo hayo kwa kiasi fulani yanachangia ligi yetu kuonekana bado inapiga hatua kurudi nyuma.
 Usajiliwa wa Oloya
Simba na Yanga zinawania saini ya kiungo mshambuliaji wa Uganda anayecheza Vietnam, Moses Oloya. Mchezaji huyu mkataba wake unamalizika oktoba lakini Simba na Yanga zinataka asitishe mkataba huo awahi kabla kipindi cha usajili wa wachezaji wa kigeni hakijamalizika mwezi Septemba.
Hata hivyo, kwa rekodi za Oloya nilizonazo sioni hadhi aliyonayo Oloya uwanjani ambayo inazifanya Simba na Yanga zimgombanie kiasi hicho na kutangaza madau makubwa. Ni straika wa kawaida sana ambaye hatofautiani na hao waliopo.  Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza wa Yanga au pale Simba Tambwe Hamis wana ubora zaidi ya Oloya ndiyo maana bado Simba na Yanga zina safari ndefu kufikia kwenye soka la ukweli. Wanafanya mambo kishabiki sana kuliko uhalisia.
Oloya kwenye ligi ya msimu huu pale Vietnam ameicheza Saigon mechi  13 amefunga mabao mawili tu. Ndiyo aina ya straika wa kigeni tunayemtaka? msimu uliopita amecheza mechi 22 amefunga mabao matatu tu. Si straika wa kugombewa kiasi hicho, tuache hizi aibu.
Tusiingie gharama ambazo haziendani na uhalisia, hivi hamjiulizi kwa nini klabu yake mpaka sasa haijamwongezea mkataba? Jibu ni rahisi tu. Ni mchezaji wa kawaida sana ambaye awepo asiwepo hana madhara, ameshindwa kazi yake lakini Simba na Yanga kwa vile zinasajili kishabiki zinamwona wa maana.
Wazungu hawawezi kumwachia mchezaji wa maana wanayemhitaji, ni kitu ambacho huwezi kukisikia popote iwe Asia au Ulaya. Simba na Yanga ambazo zinaendeshwa kishabiki ndizo zinaweza kufanya hivyo tu ndiyo maana Simba imemwachia kipa kama Juma Kaseja FC Lupopo ikamnasa. Yanga nayo ikawa haina uhakika kama inamtaka Kiiza au la mpaka dakika ya mwisho. Wanaojua mpira wanataka kumsajili ndiyo ikarudi kumpa fedha nyingi akasaini.
 Mambo yanakwenda kishabiki sana, klabu ni kongwe na zina wanachama wengi lakini hazijui zinachotaka na hazina watu weledi wanaojua kinachotakiwa kufanyika.
Klabu kuanza ligi na wagonjwa
Kwa mujibu wa TFF asilimia kubwa ya klabu za Bara hazijjawasilisha ripoti za afya za wachezaji wake. Hiyo inamaanisha kwamba wamefanya usajili bila kupima afya jambo ambalo ni hatari. Klabu inamsajili mchezaji bila kujua afya yake ikoje na ana kasoro gani, mwishowe wanakuja kuingia hasara msimu mzima kutokana na majeruhi na matatizo mengine ya kiafya. Lakini kinachonishangaza mimi ni upole wa TFF. Ilichofanya badala ya kufuata kanuni na kuziadhibu klabu ambazo zimeshindwa kutekeleza hilo wakazirudishia majina na kuziomba zirekebishe.
Umewahi kuona wapi mfumo huu wa uongozi duniani? Tutaishi kwa kuleana hivyo mpaka lini? Kwa nini zisilazimishwe kufanya mambo kitaalamu zaidi, TFF ipunguze kuleana mambo yafanywe kiutaratibu. Kutoka rohoni nawatakia ndugu zangu Waislamu Idd njema, tuko pamoja. Tanzania moja, mshikamano daima.
Chanzo Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment