Wednesday, 14 August 2013

UVCCM si moja tena, makundi kibao

Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kwa siku za karibuni inakuwa ni nadra kusikika katika harakati mbalimbali za kisiasa, ukiondoa mkutano wa karibuni wa kuzungumzia mchakato wa Katiba.
Kwa miaka ya nyuma, jumuiya hii ambayo inatajwa kama chungu cha kupika makada wa chama, harakati zao zilikuwa nyingi, za wazi na mara nyingi harakati zake zilitia joto shughuli za CCM na kuathiri hata maamuzi ya chama katika kuteua wagombea katika nafasi mbalimbali za vyombo vya dola.
Jumuiya hiyo hivi sasa imepoa, harakati zake zimetulia na inanyemelewa na mtafaruku ambao unatajwa kuwa katika sura tofauti; wapo ambao wanadai ni makundi kuelekea 2015 na wengine wakipinga kuwapo kwa hali hiyo bali wakieleza kuwa unachochewa na baadhi ya wanachama wasiotaka mabadiliko.
Wanaodai kuna makundi wanahusisha UVCCM na mbio za urais, dhana ambayo inakataliwa katakata na Mwenyekiti wa jumuia hiyo, Khamis Sadifa Juma ambaye anadai kuwa kilichopo ndani ya jumuia hiyo ni tabia ya watu kufanyakazi kwa mazoea.
Tatizo nini
Anasema ingawa vikao vipo na vinatoa maamuzi mbalimbali, lakini linapokuja suala la utekelezaji hakuna anayewajibika na matokeo yake jumuia kukosa maendeleo ya maana. “Kwa ufupi hakuna uwajibikaji,” anasema.
Mwenyekiti anasema kuwa kuna watu ndani ya jumuia hiyo ngazi ya taifa ambao wanawakwamisha watendaji wa ngazi zingine za mikoa na wilaya kutokana na ugoigoi wao kiutendaji, hali inayosababisha maamuzi mengi ya ngazi ya Taifa kutokuwafikia kwa wakati au kutokufika kabisa.
Anatoa mfano wa maamuzi ya Kamati ya Utekelezaji ya jumuiya hiyo ya kuidhinisha pikipiki 10 kupelekwa Zanzibar na nyingine tano mkoani Morogoro, kakini kwa zaidi ya miezi miwili hakukuwa na utekelezaji wa maamuzi hayo.
“Uwajibikaji kwa baadhi ya watu ndani ya UVCCM ni tatizo na hapo walitaka suala hilo liulizwe katika kikao kingine baadaye mwaka huu au mwakani wakati pikipiki hizo zipo, na mbaya zaidi nyingine zinaharibika na kuna ambazo hata funguo zake hazijulikani anazo nani,” anasema.
Anasema pikipiki hizo zipo tangu mwaka 2010 na kuna watu makao makuu wana magari na pikipiki pia, lakini kuna watendaji pale hawana hata baiskeli huku katika utekelezaji wa kazi za jumuia wanalazimika kukodi bodaboda au kupanda daladala, na hakuna anayejali.
“Kuna ambao hawajawajali wenzao wala jumuia na wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi. Na watu hao hawataki mabadiliko iwe ya kiutendaji au kiuchumi na daima wangependa kuiona jumuiya ikibaki ilipo bila kupiga hatua,” analalamika Sadifa.
Anasema mifano ipo mingi, akigusia tukio la watendaji wa jumuiya kukataa kutoa Sh14 milioni ambazo aliomba na wajumbe wengine kufanya ziara katika mikoa mitano ya Zanzibar.

“Tuliomba hela hazikutolewa, tukatumia pesa zetu na wakati tumemaliza ziara ndio tunaletewa Sh1 milioni,” anasema na kuongeza kuwa pesa kama hizo zilitumika kwa ajjili ya ziara ya mkoa mmoja tu wa bara, jambo ambalo anasema haliingii akilini.
Anasema kutokana na mifano hiyo michache ni dhahiri  kuna walakini ndani ya jumuia hiyo na lazima ufanyiwe kazi ili kuondokana na watu wachache wenye malengo binafsi.
“Watu hao wapo na wanafahamika na wao wanachofanya ni kusubiri kutumiwa na makundi ambayo yanataka rais kila unapokaribia,” anasema na kutoa onyo: “Siku zao zinahesabika nitahakikisha jumuia hii inakuwa na tija kwa vijana wote na sio watu wachache.”
“Simuogopi mtu na sikuchaguliwa uenyekiti wa UVCCM kwa bahati mbaya, bali nimepitia taratibu zote na sipo kulipa hisani za mtu au kikundi fulani cha watu,” anasema na kusisitiza kuwa mabadiliko katika jumua hiyo ni lazima na asiyeyataka achague pa kwenda.
Katibu mkuu anena
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela anasema ndani ya jumuiya hiyo kila kitu kinafanywa kwa kufuata utaratibu na maamuzi ya vikao, hivyo asingeweza kuwa na maoni zaidi yautekelezaji wa maamuzi ya vikao.
Kuhusu mgawo wa vitendea kazi kama vile pikipiki ambazo zimetolewa mfano anadai kuwa hawezi kulizungumza nje kikao husika, ingawa anakiri kuwapo kwa pikipiki 114 kabla 12 zilizochukuliwa na UVCCM Zanzibar.
“Kama kuna pikipiki zipo sioni tatizo kwani haziozi ni raslimali za jumuia na zitagawiwa kwa kufuata utaratibu na kimsingi hali ndani ya jumuia ni shwari,” anasema.
Hata hivyo kauli ya Shigela inapingana na ile ya Katibu wa Chipukizi, Omary Justus.
Justus ambaye pia ni mjumbe wa Nec anasema kuna hali isiyoeleweka ndani ya jumuiya hiyo ambayo inatokana na msimamo wa mwenyekiti wao, kukataa kuburuzwa na ‘vijana maslahi’ ambao awali waliigeuza jumuia hiyo mradi binafsi.
“Kuna watu ambao waliigeuza jumuia kama taasisi isiyo ya kiserikali (NGO) yao,” anasema na kuongeza kuwa watu hao ndio wangependa kuiona jumuiya ikiendelea kuwa tegemezi kwa wahisani na watu wanaoitwa wafadhili,” anasema Justus.
Kwa upande wake Ofisa wa UVCCM Taifa, Nkinda Lufunyo anasema msingi wa migogoro inayofukuta ndani ya jumuia hiyo ni hatua ya kiuentadaji ambayo inamfanya mchumi wa jumuia hiyo kutokuwa mmoja kati ya watu ambao wanaidhinisha malipo.
“Leo umeona wapi mchumi mkuu yupo lakini ambaye anasaini kwa ajili ya masuala ya fedha ni naibu wake, jambo hili haliingilii akilini na linakwamisha masuala muhimu ya jumuia,” anasema na kuongeza kuwa  hajui chimbuko la muundo huo.
Anasema hivi sasa kuna mizengwe inasukwa ya kutaka mwenyekiti huyo ang’oke kwa madai kuwa anaingilia utendaji wa viongozi wengine wa jumua hiyo na madai kuwa ana umri mkubwa kuliko anavyodai mwenyewe.
Hata hivyo madai yanakanushwa na mwenyekiti akidai kuwa yote hayo ni propaganda ambazo zinasukwa na wasiotaka maendeleo wala mabadiliko.
Mwananchi.

No comments:

Post a Comment