Monday, 12 August 2013

Mmarekani wa Simba: Nitafunga mabao 27

MSHAMBULIAJI wa Simba,  Betram Mombeki amesema msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unaoanza Agosti 24 anataka kufunga mabao 27 na kutwaa Kiatu cha Dhahabu.
Hakuishia hapo kwani amewaonya mabeki  wa timu pinzani kuwa makini na shughuli pevu inayokuja mbele yao.
Akizungumza na Mwanaspoti mchezaji huyo mrefu alisema msimu huu wa kwanza kwake, anataka kufanya mambo makubwa matatu ikiwamo kuiwezesha klabu yake kuchukua ubingwa, kuwa mfungaji bora na hata kuchezea Taifa Stars.
“Nafikiri unajua malengo ya timu nyingi ni kushinda ligi, pia malengo ya washambuliaji wengi ni kufunga mabao na kuwa mfungaji bora, kwa hilo naona inabidi nifanye jitihada zaidi na ninaamini ninaweza kuwa mfungaji bora na kuiwezesha klabu yangu kushiriki mashindano ya kimataifa,” alisema Mombeki anayesifika kwa mabao ya kuvizia kama Chicharito wa Man United.
“Kutokana na ushirikiano nitakaoupata kwa wachezaji wengine, nina uhakika mabeki wa timu pinzani watakuwa na kazi ngumu kwani kikosi chetu kina hamu ya ubingwa,” alisema Mombeki.
Katika hali ya kushangaza, Mombeki akaenda mbali zaidi na kuishangaa Simba kuendelea kumng’ang’ania Moses Oloya wakati kuna straika hatari Mrundi Amis Tambwe, ambaye ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao na kutoa pasi kwa mshambuliaji mwingine kufunga.
“Tambwe akianza mazoezi na kujiunga na sisi, tutafanya kazi nzuri sana kwani nimekuwa nikitazama staili yake ya uchezaji kupitia mitandao ya ‘You Tube’, nadhani mwalimu akinipa nikae naye sambamba tutafanya mambo mazuri tofauti na nikikaa na Oloya.
“Namfahamu Oloya, nilishamwona nchini Uganda siku za nyuma wakati nikisoma huko, ni mchezaji mzuri na ninaamini uwezo wake una nafasi Simba, lakini nadhani pia sisi tunaweza na tupo wengi tayari na matokeo tutayapata,” alisema Mombeki, maarufu kwa jina la Mmarekani wa Simba kwa sababu amewahi kuishi huko kwa miaka mitatu.
Kwa mujibu wa mtandao wa Shirikisho la Soka Burundi, katika msimu uliopita Tambwe aliifungia klabu yake ya Vital’O mabao 18 na akawa mfungaji bora wa Kombe la Kagame lililofanyika miezi miwili iliyopita Sudan.
Chanzo Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment