KUTOKUWA fiti kwa wachezaji wengi wa Yanga akiwamo kiungo Athuman Iddi ‘Chuji’ kumewarudisha mazoezini haraka wachezaji wa timu hiyo kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Hisani dhidi ya Azam, Jumamosi.
Yanga itaumana na Azam inayorejea leo Jumanne kutoka Afrika Kusini ambako iliweka kambi ya siku kumi na kucheza mechi tatu, huku ikishinda moja na kupoteza mbili.
Kwa kawaida, kila timu hiyo inapocheza, Kocha Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts huwapa mapumziko ya siku moja au mbili wachezaji wake, lakini imebidi afute mapumziko hayo jana Jumatatu na kuendelea na mazoezi na kikosi chake ili kukiweka fiti na kuepuka kuadhirika mbele ya Wana Lambalamba.
Habari zinadai kuwa baada ya mchezo dhidi ya SC Villa juzi Jumapili kocha huyo alionekana kulalamika kwenye vyumba vya kubadilishia nguo akiwatuhumu baadhi ya wachezaji kutokuwa fiti na kucheza chini ya viwango vyao hasa Chuji na hivyo kuwataka wachezaji wote mazoezini jana Jumatatu.
Chuji kiungo mahiri ambaye humudu kucheza namba nyingi uwanjani ikiwemo beki wa kati, kiungo mkabaji na hata kiungo mchezeshaji alijikuta akicheza kipindi kimoja tu katika mechi tatu za kirafiki alizocheza huku akionekana kutokuwa fiti.
Kiungo huyo mahiri kwa pasi ndefu maridadi zinazofika kwa walengwa na kusababisha mabao ameshindwa kuonyesha uwezo wake wa kuchezesha timu jambo ambalo Brandts amelishtukia. Brandts aliiambia Mwanaspoti kuwa wachezaji wake wengi walicheza vizuri katika mchezo huo ingawa baadhi yao hawakuwa fiti akiwamo Chuji jambo ambalo lilimlazimu kuwarudisha mazoezini kwani wana mechi ngumu Jumamosi dhidi ya Azam.
“Mechi za kirafiki zimenisaidia kuwajua vema wachezaji wangu na upungufu wao na kama unavyoona katika mchezo dhidi ya SC Villa tulitakiwa kufunga mabao mengi lakini tulikosa kuzitumia nafasi nyingi tulizopata,” alisema Mdachi huyo.
“ Bado timu haiko fiti sana kama ninavyotaka, baadhi ya wachezaji wanacheza vizuri, lakini wengine wanaonekana hawako fiti akiwamo Chuji hivyo hakuna kupumzika ni mazoezini kesho (jana Jumatatu) kwa sababu tuna mechi ngumu dhidi ya Azam na ni timu nzuri hivyo hatuwezi kukabiliana nao, nina wachezaji nusu nusu ambao wako fiti lakini nataka timu nzima iwe katika kiwango sawa tena cha juu” alisema Brandts.
Chanzo Mwanaspoti

No comments:
Post a Comment